UNESCO YAWAFIKIA VIJANA UDOM


  • 1 month
  • The University of Dodoma Hospital

Katika kuhakikisha Vijana wanamaliza safari yao ya masomo bila vikwazo, Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni- UNESCO, kupitia mradi wake wa Haki Zetu, Maisha Yetu, Mustakabali Wetu ( "Our Rights Our Lives Our Future") unaofahamika kama “O3 Plus”limeboresha mazingira ya vituo vya afya vinavyopatikana Chuoni hapo.

Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano ya vifaa iliyofanyika tarehe 27 Machi 2024, Mganga Mfawidhi Hospitali ya Chuo Kikuu cha Dodoma, Dkt. Boaz Matogolo, amesema UNESCO imewezesha kukarabati vyumba 4 vya madaktari ( vyumba vya kuona wagonjwa), kukarabati wodi 2 za wagonjwa, ukarabati wa vyoo, ununuzi wa vifaa mbalimbali kama vile mabenchi ya kisasa ya kukalia wagonjwa wakiwa wanasubiri kumuona daktari, luninga ambayo huonyesha vipindi vya afya na kuwezesha wagonjwa kupata elimu wawapo eneo hilo, pamoja na kuboresha sehemu ya mapokezi kwa wagonjwa.

Naye, Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO)Bw. Michel Toto, amesema Shirika lake linaunga mkono juhudi za Serikali na wadau mbalimbali wa elimu na afya katika kuwezesha wanafunzi kupata elimu na huduma sahihi za afya na ustawi ili waweze kustawi na kufikia malengo yao ya elimu na kuweza kuleta mchango chanya kwa Jamii na Taifa"

Naye Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma, Utafiti na Ushauri Elekezi, Prof. Razack Lokina, akizungumza kwa niaba ya Makamu Mkuu wa Chuo, amepongeza na kuishukuru UNESCO kwa msaada huo, kwa kuwa maboresho yaliyofanyika yatasaidia utoaji huduma kwa ufanisi zaidi kwa wanafunzi, wafanyakazi na wananchi wote wanaopata huduma katika Hospitali ya Chuo Kikuu cha Dodoma. Aidha, ametoa wito kwa mashirika mengine kuendelea kutoa ushirikiano kwa UDOM ili kukiwezesha Chuo hicho kuendelea kutoa huduma bora na kuhakikisha kinafikia malengo yake.

Halfa hiyo pia ilihudhuriwa na Mkurugenzi wa Elimu ya Juu kutoka Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia, Prof. Peter Msoffe, na Kaimu Mkurugenzi Idara ya Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Ahmed Makuwani, ambao wameishukuru UNESCO kwa kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuboresha huduma za afya na ustawi kwa vijana.

Comments
Send a Comment