ZOEZI LA KUGAWA VIFAA TIBA


  • 1 year
  • School of Nursing and Public Health

Waziri wa Afya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. @ummymwalimu ameongoza zoezi la kugawa vifaa tiba kwa vituo 20 vya Afya mkoani Dodoma kupitia mradi wa kuboresha huduma jumuishi za Kifua kikuu, Malaria na UKIMWI kwa Wajawazito kabla na baada ya kujifungua

Mradi huu unatekelezwa na Chuo Kikuu cha Dodoma kwa kushirikiana na Liverpool School of Tropical Medicine chini ya ufadhili wa Global Fund na Takeda Pharamaceuticals. Zoezi hili lilifanyika katika kituo cha afya cha Makole kuwakilisha vituo vingine 19 ambavyo vinashiriki katika mradi huu.

Katika hotuba yake Mhe. Ummy Mwalimu amekipongeza Chuo Kikuu cha Dodoma na Washiriki wake kwa kutekeleza mradi huu, amesema;
"Tunashukuru sana Prof. Kwa kubuni mradi huu kwa sababu ni matumaini yetu mradi utasaidia katika harakati za serikali kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi chini ya Rais wetu Dkt. Suluhu Hassan.
Mhe. Ummy Mwalimu aliwahakikishia wananchi kuwa serikali itahakikisha upatikanaji wa dawa muhimu kama dawa ya kuzuia kutoka damu wakati wa kujifungua, dawa za kuongeza damu na dawa za kuzuia kifafa cha mimba. Amewaasa watoa huduma za afya kuzingatia taaluma zao,weledi wa kazi, maadili na viapo vyao vya utumishi ili kuokoa Maisha ya wale wanao wahudumia.

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma Prof. Lughano Kusiluka amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa jinsi anavyotoa kipaumbele kwenye masuala ya Afya.

" Kipekee napenda kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya katika kuimarisha huduma za Afya katika nchi yetu na hasa katika eneo hili la mama na mtoto

"Tunashukuru kwamba katika miaka miwili ya utekelezaji wa mradi huu inaoneshwa kwamba mradi umepokelewa vizuri na matokeo yake yameanza kuonekana kwenye kiwango cha ubora" Prof Kusiluka

Aidha Mtafiti Mkuu wa Mradi Dkt. Leonard Katalambula ameeleza kua wanakusudia kuongeza idadi ya vituo vya afya, kuongeza idadi ya mikoa, kuongeza idadi ya vifaa tiba kwa vituo vitakavyo kuwa katika mradi na vilevile kuwa na kituo cha Pamoja cha mafunzo kwa vitendo kwa watumishi walioko kazini. Hivyo ameelezea jitihada za kuendelea kupata fedha kuendeleza mradi na hivyo Chuo Kikuu cha Dodoma kimeomba fedha kupitia mfumo wa ndani wa fedha za Global Fund (Country Coordinating Mechanism) ili kufanikisha hilo 

Comments
Send a Comment