KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA ELIMU, UTAMADUNI NA MICHEZO WAVUTIWA NA UWEKEZAJI MKUBWA UDOM


  • 8 months
  • Office of The Vice Chancellor

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo, tarehe 10/8/2023 ilitembelea Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa, pamoja na kupokea taarifa ya Maendeleo ya Chuo.

Kamati hiyo ilipokelewa na Naibu Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Mhe. Omar J. Kipanga na Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Dodoma, Prof. Rwekaza Mukandara, ambao kwa pamoja walitembelea miradi ya maendeleo inayoendelea kutekelezwa ukiwemo mradi wa ujenzi wa jengo la hospitali kwa ajili ya vipimo vya mionzi, kwa lengo la kuboresha huduma za kitabibu katika hospitali ya Chuo hicho.

Akizungumza mara baada ya kukamilisha ziara ya kukagua miradi, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezi, Mhe. Husna Juma Sekiboko, amepongeza jitihada kubwa za uongozi wa Chuo katika kuanzisha miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwa makusanyo ya fedha za ndani na kuitaka Serikali kupitia Wizara ya Elimu, kuangalia namna bora ya kuongezea nguvu miradi hiyo ili kukamilika kwa wakati.

Kwa hakika huu ni uzalendo mkubwa kwa Taifa, tumetembelea na kuona uwekezaji mkubwa wa jengo la hospitali kwa ajili ya vipimo vya mionzi, na ujenzi wa uzio katika eneo la nyumba 29 zilizonunuliwa na Chuo kwa ajili ya Watumishi, kwakweli miradi hii ikikamilika itakuwa na manufaa makubwa kwa wananchi hususani wakazi wa Dodoma, na wanafunzi ambao wanasomea masomo ya Afya, kutumia Hospitali hiyo kufanya majaribio kwa vitendo alisisitiza

Naye Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Omar J. Kipanga, ameishukuru Kamati hiyo kwa kutembelea UDOM, na kuahidi Wizara kwa kushirikiana na wadau wengine muhimu katika Sekta ya Maji kuendelea kufuatilia na kushughulikia changamoto ya maji iliyoanishwa kwa Kamati wakati wa ziara hiyo.

Nikuahidi Mwenyekiti, suala la maji kwa Chuo chetu nila kipaumbele, na tayari kama Wizara tulishaweka mikakati ya kushughulikia changamoto hiyo kwa kushirikisha Wizara ya Maji alisema

Akiwasilisha taarifa ya Chuo kwa Kamati, Makamu Mkuu wa Chuo Pof. Lughano Kusiluka amesema, ujenzi wa Jengo la Huduma za mionzi katika Hopsitali ya Chuo umegharimu Tshs. Bilioni 3.4 na tayari umekamilika kwa asilimia 98, na hatua inayoendelea sasa ni kufunga umeme pamoja na kuanza mchakato wa manunuzi ya vifaa na uwekaji Samani.

Aidha ameeleza ununuzi wa nyumba za watumishi umegharimu Tshs. Bilioni 2.2; huku gharama za ujenzi wa uzio zikiwa ni Tshs. Milioni 179. Fedha zote zimetokana na vyanzo vya ndani, na kwamba Menejimenti inaendelea kubuni vyanzo vipya vya mapato ili kuongeza wigo wa kukusanya mapato yatakayosaidia utekelezaji wa shughuli nyingine za maendeleo chuoni hapo kama zilivyoanishwa katika Mpango Mkakati wa Chuo.

Kamati hiyo imehitimisha ziara yake kwa kusisitiza UDOM kuendelea kuboresha eneo la Taaluma, kwa kubuni program zinazoendana na mahitaji halisi ya soko, pamoja na kukazia nidhamu kwa wanafunzi ili kuendeleza sifa nzuri ya kuwa Chuo Bora nchini Tanzania na Afrika.

Comments
Send a Comment