WATAFITI WASISITIZA UMUHIMU WA LUGHA ZA ASILIA KWA JAMII


  • 8 months
  • College of Humanities and Social Sciences

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Prof. Lughano Kusiluka, amezitaka jamii za kiafrika na hasa wale wanao tumia lugha za asili kuendelea kuthamini lugha zao na hasa kupata maarifa ya namna lugha hizo zina thamani katika kulinda tamaduni mahalia.

Hayo ameyasema jana wakati akifungua warsha ya siku tano ya watafiti kutoka nchi 9 za Afrika na Ulaya (Uingereza, Ujerumani, Israel, Kenya, Ethiopia, Zimbabwe, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Uganda na mwenyeji Tanzania), yenye lengo la kujadili na kutafiti umuhimu wa lugha za asili kwenye masuala ya kuhifadhi kumbukumbu za tamaduni za watu. Warsha inafanyika kwa siku tano kuanzia tarehe 04 hadi 08 Septemba, 2023, katika Ndaki ya Insia na Sayansi ya Jamii Chuo Kikuu cha Dodoma.

Aidha, Prof. Kusiluka ameeleza umuhimu wa kufanya tafiti na kutunza historia ya makabila 120 ya Tanzania, na kwamba tafiti zilizofanyika hadi sasa zimetupa changamoto ya kuheshimu lugha zetu, utamaduni wetu, na kwamba Chuo Kikuu cha Dodoma kitaendelea kufanya tafiti kwenye eneo hili, kwa lengo la kusaidia Serikali na Jamii kwa ujumla kutambua umuhimu wa utunzaji wa maarifa ya lugha asili, na kuendelea kuenzi mila na tamaduni zetu tulizorithi kwa mababu.

“Lengo la warsha hii ni kubalidilishana uzoefu kuhusu matumizi ya lugha katika kuhifadhi maarifa asilia na kuona kwa namna gani maarifa asilia yanaweza kutunzwa kwa ajili ya vizazi vijavyo.” Alisisitiza

Naye Mhadhiri wa lugha kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma Dkt. Chrispina Alphonce, ambaye pia ni mratibu wa warsha hiyo, amesema ni muhimu kwa jamii kujua kutumia maarifa yaliyopo katika lugha zao za asili, kwani kuna faida nyingi katika kukuza utamaduni wa jamii husika na taifa kwa ujumla.

Washiriki wa Warsha hiyo pamoja kufanya mijada ya kina ya tafiti zilizofanyika pia watatembelea mkoa wa Manyara, ambako watakutana na makabila makubwa mawili Datooga na Wairaki na kujifunza masuala mbalimbali yanayohusu namna gani wanalinda na kuenzi lugha za asili, athari za mazingira na mwingiliano wa tamaduni unavyoathiri lugha za asili, elimu, utandawazi na matibabu ya magharibi yalivyochangia makabila hayo kupoteza asili.

Matokeo ya warsha hiyo ni kuibuliwa kwa maeneo mengi zaidi ya utafiti kusaidia nchi za Afrika kulinda tamaduni na lugha za asili sambasamba na utandawazi.

Warsha hiyo imefadhiliwa na Shirika la Kimataifa la Volkswagen la nchini Ujerumani, Chuo Kikuu cha Cologne Ujerumani na Chuo Kikuu cha Dodoma.

Comments
Send a Comment