MWAKA WA KWANZA WASISITIZWA KULINDA MAADILI MEMA NA KUTUNZA HESHIMA YA CHUO


  • 6 months
  • Office of The Chancellor

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma Prof. Lughano Kusiluka amewataka wanafunzi wote wa mwaka wa kwanza kuzingatia na kuendeleza maadili yote mema na kuwajibika kulinda heshima ya chuo.

Prof. Kusiluka ameyasema hayo wakati akizungumza na wanafunzi wa mwaka wa kwanza kwenye semina elekezi iliyofanyika katika ukumbi wa Chimwaga tarehe 03, Novemba, 2023. Semina hiyo ilijumisha wanafunzi wote wa mwaka wa kwanza kutoka Ndaki, Shule Kuu na Taasisi.

Aidha Prof. Kusiluka ametoa rai kwa wanafunzi kutumia muda wao vizuri pindi wanapokuwa chuo ili waweze kufikia ndoto zao kimasomo
"Tumia muda wako vizuri ili kwanza uheshimike alafu ufaulu, uwe mtanzania ambaye nchi hii inamtamania, usome kwa bidii hakuna mteremko pale ambapo pana changamoto tupo hapa kwa ajili ya kuwasaidia"

Naye Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Prof. Razack Lokina ametoa takwimu za zoezi la udahili kuwa wanafunzi wapatao 12,845 wamechaguliwa kujiunga na chuo Kikuu cha Dodoma mwaka wa masomo 2023/24 kati ya 89,000 waliomba, pia amewataka wanafunzi wote ambao hawajajisajili wamalize usajili wao kabla zoezi halijafungwa maana hawatatambulika kama wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma.

Kwa upande mwingine Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Mipango, Fedha na Utawala Prof. Wineaster Anderson amewapongeza wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga na kuwakaribisha Chuo Kikuu cha Dodoma na kuwataka wawe watiifu kufuata sheria zote za chuo na wahakikishe usalama wao pindi wawapo chuo na pia kusisitiza kushirikiana wao kwa wao.

Semina elekezi kwa wanafunzi wa mwaka wa kwanza zinaendelea kutolewa katika ngazi ya Ndaki/ Shule Kuu na Taasisi
 

Comments
Send a Comment