VIJANA WANOLEWA KATIKA MATUMIZI YA MTANDAO


  • 3 weeks
  • The University of Dodoma

Naibu waziri wa wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Mhandisi Kundo Mathew (Mb) amewataka vijana kuendelea kuelimishana juu ya kulinda usalama wa anga na kuwa na ujuzi wa kutosha wa kulinda mifumo inayotengenezwa nchini ili kulinda uwekezaji mkubwa wa miradi ya kimkakati ya Serikali kama SGR na ujenzi wa bwawa kubwa la umeme ambayo itaendeshwa kwa mifumo ya mawasiliano ya TEHAMA.

Mhe. kundo ameyasema hayo leo tarehe 18 Novemba, 2023 wakati wa Uzinduzi wa Kampeni ya Kitaifa ya Mitandao na Vijana iliyofanyika Chuo Kikuu cha Dodoma. Kampeni hiyo inalenga kuelimisha vijana juu ya matumizi sahihi na salama ya mtandao.

“Sera yetu ya posta 2003 katika uanzishaji na makubaliano yetu ya kikanda na kimataifa ya kuwa na anuani za makazi tumeunda mfumo unaoitwa NaPA; huu ni mfumo wa kidigitali wa Anwani za Makazi na Postikodi ambao lengo lake ni kuhakikisha kila taasisi ama mwananchi anakuwa na anwani ya makazi katika eneo lake la nyumbani, ofisini ama biashara. Kinachofurahisha ni kwamba mfumo huu umetengenezwa na vijana kutoka Wizara yetu na vijana kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma nawapongeza UDOM kwa kutoa vijana bora hasa katika masuala ya TEHAMA.” alisisitiza.

Akizungumza wakati akitoa neno la ukaribisho Makamu Mkuu wa Chuo Prof. Lughano Kusiluka amesema kuwa kasi ya ukuaji wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano imeleta fursa nyingi kwa vijana ikiwa ni pamoja na kupata elimu, maarifa na ujuzi. Prof. Kusiluka ametoa rai kwa vijana kutumia mitandao vizuri kwa ajili ya maendeleo yao na Taifa kwa ujumla.

Naye mwakilishi Mkazi na Mkuu wa Ofisi ya UNESCO Tanzania Bw.Michel Toto alisema kuwa UNESCO inaendelea kuunga mkono jitihada za serikali katika mpango wa matumizi sahihi na salama ya mtandao na amewataka vijana kuongoza juhudi za kupinga vitendo vyote vya ukatili kwenye mitandao hasa kwa watoto na wanawake.

Comments
Send a Comment