WANAFUNZI WENYE MAHITAJI MAALUMU WANUFAIKA NA MRADI WA HEET


  • 1 week
  • The University of Dodoma

Ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET), Chuo Kikuu cha Dodoma kimetoa msaada wa vifaa vyenye thamani ya zaidi ya Shilingi mil 28, kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu wanaosoma chuoni hapo ili kuwasaidia kurahisisha shughuli za kitaaluma wawapo chuoni.

Hafla hiyo fupi imefanyika tarehe 6 Mei, 2024 katika ukumbi wa Seneti uliyopo jengo la Benjamin Mkapa, ikihusisha wanafunzi 163, kutoka Ndaki/Shule Kuu na Taasisi zilizopo chuoni hapo wenye ulemavu wa aina mbali mbali ikiwemo uoni hafifu, Changamoto za usikivu, ulemavu wa ngozi na ulemavu wa viungo.

Akizungumza wakati wa  kukabidhi vifaa hivyo Makamu Mkuu wa Chuo, Prof. Lughano Kusiluka, ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Mradi wa HEET, chini ya  Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, kwa kuhakikisha inatoa vifaa na mahitaji mbalimbali kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu. Amewataka wanafunzi hao kutumia vifaa hivyo vizuri na kuvitunza ili kuhakikisha vinawasaidia katika masomo yao.

“Serikali yetu inatambua kwamba watanzania wapo wengi na wana mahitaji mbalimbali na kwa kweli Rais wetu, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, anawapenda watanzania. Tunashuhudia kila mahali akifanya shughuli zake  hakosi kuzungumzia  habari ya watoto,  wanawake na watu wenye mahitaji maalumu. Lengo lake pasiwepo mtanzania mbaye ana uwezo wa kusoma kufikia elimu ya juu akakosa fursa ya kusoma kwa sababu ya changamoto za ulemavu” Alisitiza Prof. Kusiluka. 

Naye Mratibu wa Mradi UDOM, Prof. Razack Lokina, amesema mbali na vifaa hivyo, mradi huo pia utawezesha kuanzishwa kwa dawati mzunguko kwa ajili ya kutoa huduma  kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu ili kusaidia wanafunzi  na watumishi wote wenye mahitaji maalum kupata msaada wa haraka muda wote wanapokuwa chuoni. 

Akizungumza kwa niaba ya wanufaika wa vifaa hivyo Bw. Juma Said, ambaye ni mwanafunzi wa mwaka wa kwanza katika Shahada ya awali katika Elimu Maalumu ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Chuo Kikuu cha Dodoma kwa msaada huo ambao utawawezesha kufanya vizuri katika masomo yao; huku akitoa wito kwa Wanafunzi wenzake kutumia vifaa hivyo vizuri ili lengo la Serikali la kuwapatia vifaa hivyo liweze kutimia. 

Mbali na vifaa vya kumsaidia Mwanafunzi mmoja mmoja, vifaa vingine vilivyonunuliwa ni pamoja na Vitabu, kamusi, karatasi na mashine za nukta nundu, kwa ajili ya kurahisisha zoezi la ukifunzaji na ufundishaji.

Comments
Send a Comment