UDOM WATOA MSAADA BUIGIRI WASIOONA


  • 2 months
  • The University of Dodoma

Kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani 2024, siku ya tarehe 6 Machi, 2024, watumishi wanawake wa Chuo Kikuu cha Dodoma wametembelea Shule ya Msingi Buigiri Wasioona iliyopo Wilayani Chamwino- Dodoma na kutoa msaada wa mahitaji mbalimbali ikiwa ni pamoja na vifaa vya kufanyia usafi na vyakula.

Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo Mratibu wa Kitengo cha Jinsia Chuo Kikuu cha Dodoma Dkt. Lily Makalanga amesema mbali na kutoa taaluma Chuo Kikuu cha Dodoma kina wajibu wa kutoa huduma za kijamii kwa makundi mbalimbali ikiwa ni pamoja na watu wenye mahitaji maalum.

Dr. Makalanga alisisitiza kwamba katika kipindi hiki cha kuelekea maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani, wanawake wa wanakumbushwa kutimiza wajibu wao kwa jamii kama wazazi kwa ustawi wa jamii yetu.

" Tumekuja hapa leo kwa ajili ya kuwasalimia na kuwaletea zawadi naomba mpokee salamu kutoka kwa Makamu Mkuu wa Chuo pamoja na wasaidizi wake ambao wamewezesha kuwaletea zawadi hizi leo "

Naye, Mwalimu Mkuu Msaidizi wa Shule ya Msingi Buigiri Wasioona Bwn. Godfrey D. Chimulika amekipongeza Chuo Kikuu cha Dodoma kwa kuwa wadau muhimu ambao mara mara wamekuwa wakitembelea kituoni hapo na kutoa wito kwa wadau wengine kujitokeza kwa wingi kwani bado kuna mahitaji muhimu ambayo kituo hicho kinahitaji.

Kauli mbiu katika Maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani kwa mwaka 2024 ni ' Wekeza kwa wanawake: Kuharakisha Maendeleo ya Taifa na Ustawi wa Jamii "

Comments
Send a Comment