UDOM YAZINDUA KAMATI YA MALALAMIKO KATIKA KAMPASI YA NJOMBE
Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) leo, Jumatatu tarehe 8 Septemba 2025, kimezindua rasmi Kamati ya Malalamiko ya Kampasi ya Njombe katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Njombe. Kamati hiyo ina jukumu la kushughulikia malalamiko yote ya wananchi yatakayotokana na utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa chuo hicho mkoani Njombe chini ya Mradi wa HEET.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhe. Anthony Mtaka, alisema kamati hiyo ni kiungo muhimu kati ya watekelezaji wa mradi na wananchi wanaoishi jirani na eneo la ujenzi, hususan wale ambao wanaweza kuathiriwa moja kwa moja na shughuli zinazotekelezwa.
“Wajumbe wa kamati hii, majukumu yenu yanahitaji uwazi, uadilifu na kujitolea. Mtapokea malalamiko kupitia njia mbalimbali ikiwemo simu, barua pepe na mifumo mingine. Ni wajibu wenu kuchambua changamoto kwa kina na kusaka suluhisho la haki,” alisisitiza Mhe. Mtaka.
Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Prof. Lughano Kusiluka, alibainisha kuwa Kamati hiyo pia ina jukumu la kutoa elimu kwa wananchi kuhusu manufaa ya mradi na fursa zinazoweza kupatikana kupitia uwepo wa chuo hicho.
“Wananchi wanapaswa kujivunia chuo hiki kinachojengwa kwa kuwa ni chao; kitakuwa mahali pa kusomesha watoto wao. Vilevile, chuo kitazalisha vijana wenye ujuzi na maarifa ya kutosha kukabiliana na changamoto za kiuchumi,” aliongeza Prof. Kusiluka.
Uzinduzi huo umehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali na wadau wa maendeleo wakiwemo Katibu Tawala wa Mkoa, Maafisa Maendeleo ya Jamii, Mazingira na Elimu, pamoja na Wakuu wa Shule, Wenyeviti wa Mitaa na wadau wengine wa Elimu.