WANAFUNZI UDOM WATOA MISAADA KWA WAATHIRIKA WA MAFURIKO HANANG


  • 4 weeks
  • The University of Dodoma

Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma kitengo cha Udhibiti wa Maafa wametoa misaada ya kibinadamu ikiwemo nguo,taulo za kike na fedha taslimu kwa waathirika wa mafuriko yaliyotokea wilayani Hanang Mkoani Manyara na kusababisha vifo vya watu 89 pamoja na watu kupoteza makazi.

Wakizungumza katika ziara Maalumu ambapo wametembelea Maeneo yaliyoathiriwa na Mafuriko Pamoja na kutoa misaada ya kibinadamu kwa lengo la kuunga mkono juhudi za Serikali katika kurejesha matumaini mapya kwa waathirika wa mafuriko.

Kiongozi wa Wanafunzi hao kutoka UDOM, Bw. Nkuvasa Rashid, amesema kuwa wamefika wilayani Hananag kwa ajili ya mafunzo kwa njia ya vitendo lakini pia kutoa misaada ya kibinadamu ambapo wameipongeza Serikali kwa kuchukua hatua madhubuti kurejesha katika hali yake Wilaya licha ya kuathiriwa na mafuriko.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Dkt. Wilhelm Kiwango, amesema kuwa Chama cha Wadhibiti wa Maafa kutoka chuoni hapo kimefika na kujionea hali halisi ya mafuriko yaliyojitokeza pamoja na kuchukua hatua ya kusaidia waathirika ili kuamsha ari ya kujifunza jinsi ya kuwa wataalamu bora wa kudhibiti maafa.

Katibu Tawala Wilaya ya Hanang, Bw. Athumani Likeyekeye, amewapongeza wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma kwa uzalendo na kujitolea kutoa misaada ambayo inakwenda kuwanufaisha waathirika wa mafuriko moja kwa moja.
 

Comments
Send a Comment