CHUO KIKUU CHA DODOMA KUANZISHA KAMPASI MPYA NJOMBE


  • 5 months
  • Office of The Vice Chancellor

Uongozi wa Chuo Kikuu cha Dodoma, leo umekutana na kufanya mazungumzo na uongozi wa Mkoa wa Njombe, kwa lengo la kuanza ujenzi wa Kampasi Mpya, chini ya mradi wa HEET.

Akizungumza mara baada ya kuwasili Makao Makuu ya Mkoa wa Njombe, Makamu Mkuu wa Chuo, Prof. Lughano Kusiluka, aliushukuru uongozi wa mkoa kwa kuwa tayari Kampasi hiyo kuanzishwa, na kueleza kwa kina namna Chuo Kikuu cha Dodoma kimejipanga kufanya ujenzi wa Kampasi hiyo iliyotengewa kiasi cha Dola za Kimarekani 8,000,000 kupitia mradi wa Mageuzi ya Kiuchumi katika Elimu (HEET) ,unaofadhiliwa na Benki ya Dunia.

“Tumefika kufanya mazungumzo ya awali kuhusu namna mradi huu tutakavyoutekeleza kwa kushiririkiana kwa karibu na uongozi wa mkoa, na kwamba muhimu ni mkoa kutenga eneo lenye miundombinu rafiki kwa ajili ya ujenzi kuanza” alisisitiza.

Akielezea aina ya programu zitakazofundishwa kwenye Kampasi hiyo, Prof. Kusiluka amesema, tayari Chuo kimeanza kuandaa pendekezo la mitaala itakayofundishwa kwa kuendana na shughuli za kiuchumi na kimaendeleo zinazotekelezwa katika mkoa wa Njombe.

Akizungumza kwa niaba ya Uongozi wa Mkoa, Kaimu Katibu Tawala Mkoa, Bw.Lusungu Mbede, ameushukuru uongozi wa UDOM kwa kuona umuhimu wa kuanzisha Kampasi Mkoa wa Njombe, na kwamba kimekuwa kilio cha miaka mingi kwa wananchi wa mkoa huo kutamani kuwa na Chuo Kikuu ambacho kitatoa mafunzo ya muda mrefu na mfupi kwa wakazi wa Njombe na mikoa jirani, kuongeza ujuzi na ufanisi katika shughuli za maendeleo.

Katika ziara hiyo, Prof. Kusiluka aliambatana na Naibu Makamu Mkuu wa Chuo anayesimamia Taaluma, Utafiti na Ushauri, Prof. Razack Lokina, ambaye pia ni
Mratibu wa Mradi wa HEET, na Mkurugenzi wa Milki na Majengo, Injinia Stella Kyabula. Akiwa na ujumbe wake walipata fursa ya kutembelea maeneo mbalimbali
ya Mkoa wa Njombe yaliyoainishwa kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo, kulingana na vipaumbele vilivyotolewa na Wizara.

Chuo Kikuu cha Dodoma ni miongoni mwa vyuo vinavyotekeleza mradi mkubwa wa mageuzi ya kiuchumi katika Elimu (HEET), ambao unahusisha ujenzi wa
miundombinu mipya ya kufundishia na kujifunzia, maabara za kisasa, kuboresha na kuimarisha mifumo ya TEHAMA pamoja na kuongeza kasi ya matumizi ya teknolojia katika kufundisha. Mradi huu unategemewa kukamilika mwishoni mwa mwaka 2026.

Comments
Send a Comment