DAWATI LA JINSIA UDOM LAASWA KUONGEZA UMAKINI


  • 2 months
  • The University of Dodoma

Dawati la Jinsia la Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) limeaswa kuongeza umakini katika utekelezaji wa majukumu yake ya kutoa haki na usimamizi wa maswala ya
kijinsia.

Ushauri huo umetolewa tarehe 06/12/2023 na Waziri wa Katiba na Sheria Mhe, Balozi Dkt. Pindi Hazara Chana (Mb) katika hafla ya uzinduzi rasmi wa siku kumi na sita za kupinga unyanyasaji na ukatili wa kijinsia mkoani Dodoma iliyofanyika UDOM.

“Dawati la jinsia linatakiwa liongeze umakini katika kutoa Ushauri na msaada kwa wanaotoa malalamiko ya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia, pia liwe na utaratibu wa kusaidia hata kabla waathirika hawajafika kutoa malalamiko ya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia kwa kuwafikiwa walengwa wake na kuibua matukio hayo” alisema Mhe. Balozi Dkt Chana.

Akizungumza katika uzinduzi huo, mratibu wa shirika la maendeleo la watu wa Ujerumani (GiZ) na meneja wa mradi wa SAFE Bi. Katharina Keihn alisema kuwa
shirika lake linaunga mkono jitihada za Serikali za kupinga na kutokomeza ukatili na unyanyasaji wa kijinsia kupitia kituo cha msaada wa sheria cha mama Samia (Mama Samia Legal Aid).

Naye mwakilishi wa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma Prof Albino Tenge alisema kuwa, kila mwaka UDOM huadhimisha siku hizi kumi na sita za kupinga ukatili na unyanyasaji wa kijinsia, na kwa mwaka huu Shule Kuu ya Sheria wakishirikiana na Dawati la Jinsia kimejipanga kufanya shughuli mbalimbali za kisheria ikiwemo kutembelea Wilaya ya Bahi ambapo watatoa Elimu na msaada wa Kisheria kwa wananchi wa wilaya hiyo.

Comments
Send a Comment