DUWASA WAAGIZWA KUHARAKISHA UPATIKANAJI WA MAJI UDOM


  • 3 months
  • Office of The Vice Chancellor

Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb), ameiagiza Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka jijini Dodoma (DUWASA), kuharakisha upatikanaji wa Maji Chuo Kikuu cha Dodoma, pamoja na kufanya utafiti wa vyanzo vipya vya maji ili kuongeza kiwango cha maji kinachohitajika kwa siku chuoni hapo.

Waziri Aweso ameyasema hayo leo tarehe 23 Januari 2024, wakati wa ziara yake ya ufuatiliaji wa hali ya upatikanaji wa maji safi chuoni hapa.

“UDOM ni sehemu muhimu sana inayozalisha Watalaamu na Watafiti hivyo ni lazima tuonyeshe umuhimu wake. Nakuagiza Mkurugenzi wa Mamlaka ya maji safi, uhakikishe unaleta timu ya wataalamu kutafiti vyanzo vipya vya maji UDOM, pamoja na kuandaa mkakati maalumu ili kuhakikisha Chuo hiki kikubwa kinapata huduma ya maji safi itakayowawezesha kuendelea na shughuli kwa utulivu, ya kuzalisha wataalamu” alisisitiza Mhe. Aweso

Aidha, amemuahidi Makamu Mkuu wa Chuo kuendelea kusisimamia kwa karibu upatikanaji wa maji UDOM, na kwamba hatakuwa kikwazo kwa Chuo hicho kupata maji safi.

“Hiki Chuo ni lazima kiangaliwe kwa ukaribu zaidi na kiwe na laini yake maalumu ili tutatue changamoto ya maji hapa” Aliongeza Mhe. Aweso

Naye Makamu Mkuu wa Chuo, Prof. Lughano Kusiluka amesema kwa wastani, DUWASA inakipatia Chuo lita 1,172,000 kwa siku wakati mahitaji halisi ni zaidi ya lita 2,296,300. Hivyo, kiasi cha maji kinachopatikana kwa sasa ni wastani wa asilimia 51 tu.

Aidha, alizitaja baadhi ya athari ambazo Chuo inazipata moja kwa moja kwa kukosa maji safi, ikiwemo malalamiko makubwa ya wanafunzi ambayo yamekuwa yakitolewa kwa njia mbalimbali ikiwemo mitandao ya kijamii, tishio la migomo na hatari ya kutokea kwa magonjwa ya mlipuko.

Mheshimiwa Aweso katika ziara hiyo alimbatana na Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma Prof. Davis Mwamfupe, Uongozi wa Juu wa DUWASA NA RUWASA, Wakandarasi na Uongozi wa Wilaya ya Dodoma.

Alihitimisha ziara yake kwa kutembelea mabweni ya wanafunzi na kuzungumza na wawakilishi wa Wanafunzi katika Ndaki ya Elimu ambako changamoto ya maji ni kubwa, pamoja na kukagua chanzo cha maji cha Iyumbu, na visima vya kuhifadhia maji vilivyoko chuoni hapo.
 

Comments
Send a Comment