KUSILUKA AGUSWA NA USHINDI MNONO WA UDOM KWENYE MASHINDANO YA "TUSA" TANGA


  • 3 months
  • Office of The Vice Chancellor

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Prof. Lughano Kusiluka, amekutana na timu ya wanafunzi 103 waliowakilisha Chuo Kikuu cha Dodoma kwenye mashindano ya michezo ya Vyuo Vikuu Tanzania (TUSA), yaliyofanyika kuanzia tarehe 13 hadi 21 Disemba, 2023 mkoani Tanga. Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kilipata ushindi mkubwa katika mashindano hayo kwa kuibuka na ushindi wa Makombe 13 na Medali 15, katika michezo 16 iliyoshiriki.

Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa ushindi huo, Prof. Kusiluka amesema amefurahishwa sana na jitihada kubwa zilioonyeshwa na timu zilizoshiriki na hasa nidhamu wakati wote wa mashindano.

Ameahidi Menejimenti kuendelea kufadhili michezo na mashindano mbalimbali ya ndani na nje ya nchi, ili kuinua vipaji vya wanafunzi katika michezo, pamoja na kuendelea kujenga na kuimarisha afya za wanafunzi katika kipindi wanachokuwa masomoni.

“Tutaendelea kutenga bajeti ya kuwezesha timu za Wanafunzi kushiriki kwenye mashindano mbalimbali zikiwemo mechi za kirafiki za ndani ili kuwatayarisha wanafunzi wetu kwa mashindano yajayo”. Alisisitiza Prof. Kusiluka

Naye Mkurugenzi wa Huduma za Wanafunzi Bi. Rhoda Aroko, amesema katika mashindano yaliyofanyika Tanga, Chuo Kikuu cha Dodoma kilishiriki michezo 16, ukiwemo mchezo wa Mpira wa Miguu, Mpira wa Pete, Mpira wa Kikapu, Mpira wa Wavu, Mpira wa Mikono, Riadha, Mpira wa Meza (Tennis), Mpira wa Mbao (Wood ball), Chesi, Pool Table na mingineyo.

Hafla ya kukabidhiwa ushindi huo ilifanyika katika ukumbi wa Midland, Dodoma, na ilihudhuriwa na Menejimenti ya Chuo, Uongozi wa Serikali ya Wanafunzi, Wanafunzi 103 waliowakilisha chuo kwenye mashindano, na wadau wengine wa michezo wa Chuo Kikuu cha Dodoma.
 

Comments
Send a Comment