UDOM WAZINDUA BARAZA LA TANO LA WAFANYAKAZI


  • 3 months
  • The University of Dodoma

Chuo Kikuu cha Dodoma kimezindua Baraza la Tano la Wafanyakazi. Uzinduzi huo wa Baraza
umekwenda sambamba na uzinduzi wa Mkataba wa Utendaji uliokabidhiwa na Kamishna wa
Kazi Msaidizi, Bw. Andrew Mwalwisi kwa niaba ya Kamishna wa Kazi.
Akizungumza kabla ya kuzindua Baraza hilo, Kamishna Msaidizi amepongeza Uongozi wa Chuo,
Vyama vya Wafanyakazi na Watumishi kwa kuona umuhimu wa kuwa na Baraza la Wafanyakazi.
Chuo pia kilipongezwa kwa kuwa mfano wa kuigwa kwa vyuo vingine ambavyo havijaweza
kufikia hatua hiyo.


Aidha, amewapongeza viongozi wote walioteuliwa kuongoza Baraza hilo kwa nafasi ya Katibu,
Katibu Msaidizi, Kamati Kuu, na Wajumbe wote wa Baraza waliochaguliwa na Mkutano wa
Kwanza uliofanyika Jumatano tarehe 01 Februari, 2024.


Kamishna Msaidizi amewataka Wajumbe wa Baraza ambao ni wawakilishi wa Wafanyakazi
kutimiza wajibu wao kwa kuzingatia Miongozo, Kanuni na Taratibu za uendeshaji wa Mabaraza
ya Wafanyakazi. Pia, amewataka Wajumbe kuhakikisha wanatumia vema nafasi zao
kuwawakilisha Wafanyakazi waliowachagua na kuwa daraja bora kati ya Menejimenti na
Wafanyakazi. Halikadhalika, amewaasa Wajumbe kuhakikisha Baraza linakuwa ni chombo cha
kuleta maendeleo na tija kwa Wafanyakazi na Taasisi kwa ujumla.


Akimkaribisha Mgeni Rasmi, Makamu Mkuu wa Chuo na Mwenyekiti wa Baraza hilo
Prof. Lughano Kusiluka, alieleza namna Menejimenti ya Chuo ilivyojipanga kushirikiana na
Wajumbe walioteuliwa katika kuhakikisha Baraza linakuwa chombo cha kuleta amani na
Mshikamano miongoni mwa wafanyakazi.


Kabla ya Hafla ya Uzinduzi, kikao hicho kilitanguliwa na mafunzo kuhusu, “Wajibu na Majukumu
ya Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi kwa Mujibu wa Sheria na Kanuni Zilizoanzisha
Mabaraza ya Wafanyakazi; Uendeshaji na Ushiriki wa Vikao na Masuala Mengine Yanayohusu
Haki na Wajibu wa Wajumbe”.

Comments
Send a Comment