UDOM KINARA MASHINDANO YA USALAMA MITANDAONI "CYBER CHAMPIONS"


  • 3 months
  • The University of Dodoma

Chuo Kikuu cha Dodoma kimeibuka Mshindi wa Kwanza katika Shindano la Tano la Usalama Mtandaoni 2023/24 "Cyber Champions", linaloratibiwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).Shindano hilo lilijumuisha washiriki 705 kutoka vyuo 41 vya taasisi za Elimu ya Juu nchini, ambapo kati ya washiriki Hamsini (50) waliofanikiwa kufikia hatua ya fainali UDOM ilitoa washiriki 31. Washiriki watatu kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma wameibuka washindi wa shindano hilo kwa mwaka 2024.

Shindano hilo lililoandaliwa na TCRA kwa lengo la kukuza uwezo kwa vijana, kuimarisha na kukabili vihatarishi vya usalama mtandaoni, limefanyika Ijumaa tarehe 2 Februari 2024 katika Ndaki ya Sayansi za Komputya na Elimu Angavu Chuo Kikuu cha Dodoma.

Akizungumza katika hafla hiyo wakati wa utoaji wa vyeti kwa washiriki hamsini (50) wa mashindano hayo, Meneja wa Mamlaka ya Mawasiliano Kanda ya Kati Mhandisi Asajile John amekipogeza Chuo Kikuu cha Dodoma kwa ushindi huo mkubwa na pia ametoa wito kwa vijana wengi kujitokeza kwa wingi kushiriki mashindano hayo kwani yanawapatia ujuzi na maarifa mapya jinsi ya kulinda usalama kwenye mitandao kwa maendeleo yao na nchi kiujumla.

Naye Kaimu Rasi wa Ndaki ya Sayansi za Komputya na Elimu Angavu, Dkt.Florence Rashid, amewapongeza wanafunzi wote walioshiriki mashindano hayo kwa kuipeperusha vyema bendera ya Chuo Kikuu cha Dodoma na ameahidi kuwa kwenye mashindano mengine wataendelea kufanya vizuri na kurudi na ushindi mnono.

Amesema kwa kuwa idadi ya washiriki wanawake ilikuwa ni ndogo hivyo ametoa wito kwa wanafunzi wa kike kujitokeza bila kuugopa kwenye mashindano mengine yoyote.

Comments
Send a Comment