HOSPITALI YA UDOM YAPONGEZWA KWA KUWA CHANZO CHA UCHUJAJI DAMU KANDA YA KATI


  • 2 months
  • The University of Dodoma Hospital

Kaimu Mkurugenzi Idara ya Tiba Wizara ya Afya Dkt. Mwinyikondo Juma Amir aliyemwakilisha Katibu Mkuu Wizara ya Afya ameipongeza Hospitali ya Chuo Kikuu cha Dodoma na kukumbuka mchango wake mkubwa kama Hospitali ya kwanza Kanda ya kati kutoa huduma za uchujaji wa damu kwa wagonjwa wa figo mwaka 2013.

Hayo yamesemwa leo tarehe 20 Februari, 2024 na Dkt. Mwinyikondo alipokuwa akizungumza katika hafla ya makabidhiano ya msaada wa vifaa tiba kutoka Taasisi ya AL NMAA Society na African Relief and Community Development iliyofanyika katika Hospitali ya Chuo Kikuu cha Dodoma.

“Wizara inatambua kwamba Hospitali hii ya Chuo Kikuu cha Dodoma ndio waanzilishi wa huduma ya uchujaji wa damu kwa wagonjwa wa figo Kanda ya Kati, hiki ndio kituo cha kwanza kutoa huduma hiyo ambacho kilifunguliwa rasmi mwezi Februari, 2013” alisistiza Dkt. Mwinyikondo.

Dkt Mwinyikondo amepongeza juhudi zinazofanywa na Chuo Kikuu cha Dodoma katika sekta ya afya kwa kutoa elimu na huduma kwa jamii huku akitoa wito kwa watumishi wa Hospitali kutunza vifaa tiba hivyo na kuvitumia katika kufanya tafiti zitakazotatua changamoto za afya katika jamii yetu.

Naye, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma Prof. Lughano Kusiluka ameishukuru Wizara ya Afya kwa kuipandisha Hospitali ya Chuo Kikuuu cha Dodoma kufikia hadhi ya Hospitali ya Wilaya. Aliongeza kuwa Chuo kinaunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya sita za kuboresha sekta ya afya nchini kwa kujipanga kuifanya Dodoma kuwa jiji ambalo litapokea watalii katika sekta ya afya.

Prof. Kusiluka alieleza kuwa Chuo Kikuu cha Dodoma ni kitovu cha kuanda Madakatari,Wauguzi na watalaamu wengine na kuahidi kuwa Chuo kitaendelea kuboresha huduma zake na kuendelea kushirikiana kwa ukaribu na serikali pamoja na wadau wengine ikiwa ni pamoja na Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Benjamin Mkapa ili kuhakikisha watanzania wanapata huduma ya afya ya uhakika.

Mkurugenzi wa Kanda kutoka Taasisi ya African Relief and Community Development and AL NMAA Society Bw. Mohamed Gewily ameshukuru kwa mashirikiano na Chuo Kikuu cha Dodoma na kuahidi kuwa wataendelea kutoa misaada mingi zaidi nchini Tanzania kuliko nchi nyingine.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Chuo Kikuu cha Dodoma Dkt. Matobogolo Boaz ameshukuru kwa msaada huo kwani utarahisisha utoaji wa huduma kwa watumishi, wanafunzi pamoja na jamii inayozunguka Chuo Kikuu cha Dodoma. Ameeleza kuwa vifaa hivyo vimegawanyika katika makundi mbalimbali ikiwa ni pamoja na vifaa tiba, vitenganishi vya maabara, vichukua sampuli, vifaa vya mazoezi na vitanda maalumu vya umeme ambavyo kwa ujumla vimegharimu Dola za Kimarekani laki 588. Dkt Matobogolo pia ametoa wito kwa wadau

wengine kujitokeza kuunga mkono juhudi za serikali katika kuhakikisha kuwa huduma za afya zinatolewa kwa ufanisi mkubwa. Katika hafla hiyo Dkt. Thea Mtara ambaye ni mbunge wa Vyuo Vikuu na Taasisi za Elimu ya Juu aliunga mkono juhudi za wadau wa maendeleo kwa kutoa msaada wa shuka 50 kwa Hospitali ya Chuo Kikuu cha Dodoma.

Comments
Send a Comment