UDOM YASAINI HATI YA MAKUBALIANO NA KITUO CHA URITHI WA UKOMBOZI WA BARA LA AFRIKA
Chuo Kikuu cha Dodoma kwa kushirikiana na Kituo cha Urithi wa Ukombozi Bara la Afrika kilichopo chini ya Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo tarehe 12 Septemba, 2024 katika Ukumbi wa Baraza la Chuo Kikuu Cha Dodoma wamesaini hati ya Mkataba wa Makubaliano wenye lengo la kuchagiza matokeo chanya ya ukombozi wa kifikra kwa vijana ndani ya Bara la Afrika.
Akizungumza katika hafla hiyo Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Prof. Lughano Kusiluka, ameishukuru Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa uamuzi wake wa kushirikiana na UDOM kwa kulinda, kuhifadhi na kutangaza Urithi wa Bara la Afrika na kwamba uamuzi huo umekuwa wakati muafaka ambao Dunia imetawaliwa na utandawazi, kiasi cha kufanya vijana wengi kupoteza utambulishio wao na historia ya nchi zao.
Ameahidi kuwa kupitia Ndaki ya Insia na Sayansi za Jamii ( CHSS) mkataba huo unatekelezwa kwa vitendo ikiwemo kuanzisha mitaala yenye kutoa mafunzo kuhusu Historia ya Tanzania.
Naye; Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Utamaduni Wizara ya Utamaduni na Michezo Bw. Mfaume Saidi, Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu amesema, lengo kuu la mashirikiano baina ya Kituo na UDOM ni kufikia kundi kubwa la vijana katika nyanja zote za kiutendaji, ili kuwezesha jitihada za ukombozi wa kifikra kwa vijana ndani ya bara la Afrika, pamoja na kufanya utafiti utakaowezesha Taifa kuwa na mikakati ya kuenzi, kulinda na kutunza Historia za waasisi.
Kaimu Naibu Makamu Mkuu wa Chuo, Taaluma, Utafiti na Ushauri elekezi, Prof. Ismail Juma Ismail, amesema mashirikiano hayo yatawezesha jitihada za ukombozi wa kifikra kwa vijana ambapo maeneo kumi na moja yatatiliwa mkazo ikiwemo kuandaa miradi ya urithi wa ukombozi wa bara la Afrika, kutoa mafunzo kwa vijana, kuandaa machapisho, kutoa ushauri elekezi, kulinda, kuhifadhi na kutangaza urithi wa ukombozi wa bara la Afrika, Utafiti, kuanzisha programu mpya na kutoa ufadhili kwa vijana.