UDOM YAWEZESHA WALIMU 674 KUBORESHA UBORA WA ELIMU
Chuo Kikuu cha Dodoma kimeanza kutoa mafunzo ya siku nne kuanzia leo tarehe 25 hadi 28 Aprili 2025 katika Shule ya Sekondari St.Margaret iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Igunga- Tabora kwa walimu wanaofundisha Hisabati na Masomo ya Sayansi kupitia mradi unaofadhiliwa na UNICEF uliojikita Kuimarisha Viwango vya Ujifunzaji na Ufundishaji wa Hisabati na Masomo ya Sayansi kwa Shule za Sekondari katika Mikoa ya Tabora, Kigoma na Songwe.
Akizungumza wakati wa Ufunguzi wa Mafunzo hayo; Kaimu Rasi wa Ndaki ya Elimu Dkt. Abdallah Seni amesema kuwa watatoa mafunzo kwa walimu 674 wa Sekondari waliotoka katika Mikoa ya Tabora, Kigoma na Songwe huku akisitiza kuwa maarifa wanayoongezewa yatumike vyema ili kuboresha ufundishaji wa Hisabati na masomo ya Sayansi, ikiwemo matumizi ya TEHAMA na mbinu shirikishi zinazozingatia jinsia kwa lengo la kuwavutia wanafunzi, hasa wasichana.
Naye; Mwakilishi kutoka UNICEF Bi. Farida Sebarua amekipongeza Chuo Kikuu cha Dodoma kwa usimamizi mzuri wa mradi huo huku akiahidi kuwa UNICEF inaendelea kushirikiana na UDOM ili kuunga mkono juhudi za Serikali zilizopo kupitia Mpango wa Uboreshaji wa Ubora wa Elimu ya Sekondari ( SEQUIP) unaojumuisha mikoa yote ya Tanzania.
Mafunzo hayo ni awamu ya tatu ambapo kwa mara ya kwanza yalifanyika mwaka jana katika wilaya ya Kasulu-Kigoma , Vwaw- Songwe na sasa ni Igunga- Tabora na hadi sasa kufikia idadi ya jumla ya walimu 1,744.