UDOM YAPIGA HATUA MRADI WA AFYA YA MAMA MJAMZITO KWA KUTUMIA AI


  • 3 days
  • The University of Dodoma

Katika Hatua za Utekelezaji wa Mradi wa AI 4 Maternal Health, Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kimefanya warsha fupi ya uwasilishaji wa Takwimu za Utambuzi wa Hatari zinazowakabili Mama wajamzito zenye Lengo la Kuboresha huduma za afya ya uzazi kupitia matumizi salama na yenye maadili ya Akili Unde (AI).

Warsha hiyo imefanyika tarehe 28 Aprili 2025, katika Ukumbi wa Afrika ya Mashariki uliopo Ndaki ya Sayansi za Kompyuta na Elimu angavu (CIVE), na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wa sekta ya Afya ikiwemo watafiti wa Mradi kutoka UDOM, Wizara ya Afya, TAMISEMI pamoja na Watumishi wa sekta hiyo kutoka wilaya za Meatu, Chamwino, Mkuranga, Kilolo, na Mbulu ambako Takwimu hizo zilikusanywa.

Akizungumza wakati wa Ufunguzi wa Warsha hiyo, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo – Taaluma, Utafiti na Ushauri Elekezi, Prof. Razack Lokina ametumia fursa hiyo kuiomba serikali kupitia Wizara ya Afya pamoja na TAMISEMI kuwaunga mkono watafiti wa Mradi huo kwa kuwa unakuja kusaidia kupunguza vifo vitokanavyo na athari za ujauzito.

Kwa upande wake Kiongozi Mkuu wa Mradi huo, Dkt. Rukia Mwaifunyi, ambaye pia ni Mhadhiri na Mtafiti Chuo Kikuu cha Dodoma, amesema kuwa Mradi huo ulijikita katika kukusanya taarifa za wamama wajawazito pindi wanapo kwenda Kliniki ambapo baadae utatengeneza mfumo utakaosaidia kugundua vihatarishi ambavyo mama mjamzito anaweza akavipata wakati wa kujifungua au baada ya kujifungua.

Mradi huo ulizinduliwa Mwezi Machi, 2024 kwa ufadhili wa LACUNA FUND na hadi sasa umefanikiwa kwa asilimia 88 huku Takwimu 8,870 za mama wajawazito zimekusanywa kutoka katika wilaya 5 nchini. Kwa Kupitia Takwimu hizo, wataalamu na watunga sera wanatarajia kuunda mfumo utakaoweza kutabiri na kudhibiti hatari zinazohusiana na afya ya mama mjamzito hapa nchini.

Comments
Send a Comment