UDOM NA URUSI WAADHIMISHA MIAKA 80 TANGU KUKAMILIKA VITA KUU YA DUNIA
Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kwa kushirikiana na Kituo cha Sayansi na Utamaduni wa Urusi nchini Tanzania, leo Mei 6, 2025 wameadhimisha miaka 80 tangu kumalizika kwa Vita Kuu ya Pili ya Dunia mwaka 1945.
Akizungumza katika ufunguzi wa hafla hiyo iliyofanyika katika ukumbi wa Chimwaga, Dodoma, Mwakilishi wa Makamu Mkuu wa Chuo (UDOM) Prof. Razack Lokina amesema tukio hili litawasaidia vijana kujifunza umuhimu wa kuenzi historia, utulivu na kudumisha amani iliyopo.
Kwa upande wake, Mtayarishaji wa Maudhui kutoka Chaneli ya Kimataifa ya “Russia Today” Bi. Viktoria Statohina, amesema, vita ina athari kubwa sana kwa jamii na kutolea mfano kwamba yeye alimpoteza babu yake vitani.
"Maisha ya dunia hayajapangiliwa kwa namna ile tunayoitaka, tunapaswa kujiuliza swali moja, tunaishi kwa makusudi gani?" Aliuliza Bi. Viktoria”.
Naye, Mtoto wa Hayati Baba wa Taifa, Bw. Madaraka Nyerere amesema Tanzania inatambua mchango wa Urusi katika harakati za Waafrika kupigania uhuru wao kutoka kwa wakoloni.
Maadhimisho hayo yameenda sambamba na onesho la filamu, picha za historia pamoja na mada kuhusu sababu, matokeo na athari za Vita ya Pili ya Dunia.