WANAFUNZI BIHAWANA SEKONDARI WAHAMASISHWA KUSOMA VITABU


  • 1 day
  • The University of Dodoma

Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kupitia Kurugenzi ya Maktaba, tarehe 29 Aprili, 2025 wametembelea Shule ya Sekondari Bihawana iliyopo jijini Dodoma, lengo likiwa kuwajengea wanafunzi ari ya kusoma vitabu pamoja na kuwahamasisha kujiunga na Masomo ya Elimu ya yanayotolewa na Chuo Kikuu cha Dodoma.

Akizungumza katika hafla iliyofanyika shuleni hapo, Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Maktaba UDOM Dkt. Rex Kidyalla, amesema UDOM ina programu zaidi ya 150, mazingira mazuri ya kujifunzia, uhakika wa Mabweni ya wanafunzi kulala, pamoja na viwanja mbalimbali vya michezo.

"Kusoma ni muhimu sana, usiposoma kwa bidii utashindwa kwenda mbele. Soma kwa bidii ili uweze kufika mbali," ameongeza Dkt. Kidyalla.

Kwa upande wake Mkuu wa Shule ya Sekondari Bihawana, Dkt. Frank Winfrid Masome, amewashukuru wafanyakazi wa UDOM kwa kuwatembelea shuleni hapo na kuahidi kwamba watahakikisha wanafunzi wanafanya vizuri darasani ili waweze kujiunga na UDOM.

Naye, Kiranja Mkuu wa Shule ya Sekondari Bihawana Bw. Joshua Lwiza John amesema ujio wa UDOM shuleni hapo umemfanya atamani kusoma programu ya Ualimu, pindi atakapomaliza masomo yake ya kidato cha sita.

Hafla hii imeenda sambamba na ugawaji wa zawadi mbalimbali kama vile vitabu vya Historia, Jiografia, Kilimo, Kiswahili na Kiingereza, kalamu, madaftari, vipeperushi vinavyoelezea programu zinazotolewa UDOM pamoja na huduma za Maktaba.

Comments
Send a Comment