WANAFUNZI WAASWA KUWEKA BIDII KWENYE MASOMO YA SAYANSI


  • 1 month
  • The University of Dodoma

Chuo Kikuu cha Dodoma kupitia Ndaki ya Sayansi Asilia na Hisabati, wametembelea Shule ya Sekondari ya Wasichana Bunge mkoani Dodoma, lengo likiwa kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Wanawake na Wasichana katika Sayansi, leo Februari 11, 2025.

Akizungumza katika hafla fupi iliyofanyika shuleni hapo, Mwakilishi wa Rasi wa Ndaki ya Sayansi Asilia na Hisabati na Mkuu wa Idara ya Biolojia UDOM Dkt. Naza Mbaga amesema, kuna fursa nyingi sana kwenye masomo ya sayansi, ambazo zitawawezesha kuweza kujiajiri au kuajiriwa.
"Someni kwa bidii, kwani unaweza kuwa mtu yeyote yule unayetaka kuwa," ameongeza Dkt. Mbaga.

Naye, Mratibu wa tukio hili Dkt. Rehema Ulimboka kutoka UDOM, amewataka wanafunzi hao kuonesha uwezo wao kwenye gunduzi na bunifu katika masomo ya sayansi, pamoja na kuhakikisha wanapata ufaulu ya daraja la kwanza.

Kwa upande wake Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Bunge Bi. Salome Mkombola amewashukuru wahadhiri kutoka UDOM kwa kuwatembelea na kuwaasa wanafunzi kuzingatia ushauri waliopewa.

Mwanafunzi wa kidato cha tano tahasusi ya Fizikia, Kemia na Hisabati (PCM) Bi. Fidea Chanai amesema, wao kama wanafunzi watajitahidi kufanyia kazi ushauri waliopewa, ili wazidi kuwa bora kwenye masomo ya sayansi.

Chuo Kikuu cha Dodoma kimepanda miti shuleni hapo pamoja na kugawa sabuni za kunawia mikono na za kusafishia vyoo, zilizotengenezwa na wanafunzi wa masomo ya sayansi kutoka Ndaki ya Sayansi Asilia na Hisabati UDOM.

Comments
Send a Comment