UDOM MWENYEJI KONGAMANO LA JUMUIYA YA LUGHA AFRIKA MASHARIKI


  • 18 hours
  • The University of Dodoma

Naibu Makamu Mkuu, Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) anayeshughulikia Taaluma, Tafiti na Ushauri Elekezi Prof. Razack Lokina, leo tarehe 13, Agosti 2025 amefungua rasmi Kongamano la 4 la Jumuiya ya Lugha Afrika Mashariki katika ukumbi wa LRB -106 uliopo Ndaki ya Sayansi za Kompyuta na Elimu Angavu.

Akizungumza katika hafla ya ufunguzi, Prof. Lokina amesema kongamano hilo linakwenda sambamba na mabadiliko ya Sayansi na Teknolojia yanayoendelea duniani kwa sasa na mjadala utajikita katika namna lugha inavyoweza kutumika katika kuchangia maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
“Dunia ipo katika uchumi wa kidijitali zaidi na inategemea lugha katika maendeleo yake, sisi kama UDOM ni fursa kwetu katika kuitangaza nchi yetu pamoja na kukitangaza chuo chetu.” Aliongeza Prof. Lokina.

Kwa upande wake Mratibu wa Kongamano hilo, Dkt. Chrispina Alphonce ambaye pia ni Mhadhiri Mwandamizi UDOM, amesema lengo la kongamano hilo ni kusaidia katika kuwaunganisha watafiti wa lugha kutoka nchi mbalimbali za Afrika na kujadili mchango wa lugha katika kuleta maendeleo.

Naye, mmoja ya washiriki katika kongamano hilo kutoka nchini Kongo (DRC), Bw. Jean-Baptiste Grodya Musafiri, ameishukuru Menejimenti ya Chuo Kikuu cha Dodoma UDOM kwa maandalizi mazuri na kukiri kuwa ushiriki wake umempatia fursa za kukutana na watafiti wabobevu kutoka UDOM.

Kongamano hilo limeratibiwa na Idara ya Lugha za Kigeni na Fasihi kutoka Ndaki ya Insia na Sayansi za Jamii UDOM, litadumu kwa muda wa siku 3 likihusisha Wanataaluma zaidi ya 250 kutoka katika nchi 25 za Afrika, Watumishi kutoka Idara mbalimbali pamoja na Wanafunzi wa Shahada za Juu UDOM.

Comments
Send a Comment