KAMATI YA BUNGE UGANDA YAVUTIWA NA MIUNDOMBINU UDOM


  • 1 week
  • The University of Dodoma

Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa, ya Bunge la Uganda imeipongeza Serikali ya Tanzania kwa uwekezaji mkubwa iliyofanya katika ujenzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma, pamoja na kusifu Amani na Utulivu mkubwa uliopo, kwa kuzingatia idadi kubwa ya wanafunzi wanaosoma chuoni hapo.

Pongezi hizo zimetolewa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Gilbert Olanya, wa Jimbo la Kilak Kusini, Alhamisi tarehe 18 Aprili 2024, walipofanya ziara ya kutembelea maeneo mbalimbali ya chuo hicho pamoja na kufanya mazungumzo na Makamu Mkuu wa Chuo, Prof. Lughano Kusiluka, kwenye ofisi yake iliyopo jengo la Benjamin Mkapa, Dodoma.

Aidha, wamevutiwa na aina ya masomo yanayofundishwa katika Ndaki, Shule Kuu na Taasisi za Chuo, pamoja na namna chuo kinavyoendelea kuwekeza katika kuanzisha programu mpya za masomo zinazoakisi mabadiliko makubwa ya kisekta yanayozingatia utoaji mafunzo wenye kutatua changamoto kubwa za ajira, na matumizi ya teknolojia katika ufundishaji.

Akiukaribisha ujumbe huo, Makamu Mkuu wa Chuo, Prof. Kusiluka amelishukuru Bunge la Tanzania kwa kuona umuhimu wa kuwaleta wabunge hao kuja kujifunza UDOM, na kueleza ni kwa namna gani wabunge hao wana mchango mkubwa katika kuongeza hamasa ya ufundishaji wa lugha ya Kiswahili katika Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, na kutunga Sera zenye kusaidia nchi hizo kuendana na mabadiliko makubwa ya kisanyansi na teknolojia katika Sekta ya Elimu.

Aidha, amewahamasisha waganda kuja kusoma Tanzania kutokana na uwepo wa mitaala mizuri na masomo yenye kukidhi mahitaji katika soko la Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla.

“Tunayo fursa ya wananchi wa Uganda na nchi nyinginezo za Afrika Mashariki kuja kusoma UDOM. Niwahakikishie tunayo mazingira mazuri na thabiti ya kujifunzia kwa wana Afrika Mashariki kuja kusoma Tanzania. Mazingira yetu, tamaduni na mahitaji yetu yanafanana, kwangu mimi hii ni fursa kwetu sote” alisisitiza

Wajumbe wengine wa Kamati hiyo waliofika kutembelea Chuo Kikuu cha Dodoma ni pamoja na Mhe. Betty Ethel Naluyima, Mhe. Dkt. Isingoma Patrick Mwesigwa, Mhe. Rwemulikya Ibanda Gerald, Mhe. Patrick Ocan na Mhe. Lillian Obiale Paparu.

Comments
Send a Comment