UDOM YAZINDUA MAFUNZO YA MRADI WA KIMATAIFA WA AI KUBORESHA HUDUMA ZA ULTRASOUND KWA WAJAWAZITO
Mafunzo ya ukusanyaji wa takwimu kwa ajili ya mradi wa “AI-Assisted Ultrasound Feasibility and Assessment of Resources and Integration (SAFARI)” yameanza rasmi Jumatatu, tarehe 30 Machi 2026, na yanatarajiwa kuhitimishwa tarehe 1 Aprili 2026. Mafunzo hayo yanafanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Ndaki ya Biashara na Uchumi (CoBE Boardroom), katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).
Mradi huu unafadhiliwa na Gates Foundation na kutekelezwa na Chuo Kikuu cha Dodoma kwa kushirikiana na Liverpool School of Tropical Medicine (LSTM), kwa kushirikisha wataalamu toka Wizara ya Afya Tanzania. Lengo kuu la mradi huu ni kufanya Utafiti na tathmini ya majaribio ya matumizi ya teknolojia ya Akili Unde (AI) katika huduma za ultrasound ili kuboresha huduma za afya kwa kina mama wajawazito nchini, na kupunguza vifo vya mama na mtoto.
Kupitia utekelezaji wa mradi huu, wataalamu wa afya wanatarajiwa kunufaika kwa kuongeza usahihi wa uchunguzi wa kitabibu, kuboresha ufanisi wa utoaji huduma, pamoja na kupanua wigo wa upatikanaji wa huduma bora za afya, hasa katika maeneo vijijini yenye changamoto ya uhaba wa Vifaa tiba na wataalamu.
Chuo Kikuu cha Dodoma kinaendelea kujidhihirisha kama kitovu cha ubunifu na ushirikiano wa kimataifa, kikilenga kuimarisha afya ya mama na mtoto pamoja na kuchochea maendeleo ya sekta ya afya nchini Tanzania.