UDOM YASHIRIKIANA NA WIZARA YA AFYA KUANDAA MUONGOZO WA MATUMIZI YA AKILI UNDE KATIKA HUDUMA ZA SONOGRAFIA (ULTRASOUND)
Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), kupitia Shule Kuu ya Uuguzi na Afya ya Jamii (SoNPH), kwa kushirikiana na Wizara ya Afya Tanzania, kimewakutanisha wadau wa sekta ya afya nchini kujadili na kuandaa muongozo wa matumizi ya Akili Unde (AI) katika huduma za sonografia (ultrasound), hususan kupitia teknolojia ya Point of Care Ultrasound (POCUS).
Kikao hicho kilichofanyika Morogoro kimehusisha wadau mbalimbali wakiwemo wawakilishi kutoka Ofisi ya Rais – TAMISEMI, mabaraza ya kitaaluma, vyama vya kitaaluma, vituo vya kutolea huduma za afya pamoja na vyuo vikuu. Lengo kuu lilikuwa kujenga uelewa wa pamoja na kuweka miongozo itakayosaidia matumizi sahihi, salama na yenye tija ya teknolojia hiyo katika ngazi zote za utoaji huduma za afya, hasa katika vituo vya msingi.
Akizungumza wakati wa kikao hicho, Mhadhiri na Mtafiti Mkuu wa mradi huo kutoka UDOM, Dkt. Leonard Katalambula, alieleza kuwa juhudi hizo zinalenga kuimarisha ushirikiano wa wadau na kuweka msingi thabiti wa matumizi ya POCUS katika kuboresha huduma za afya nchini.
Kwa upande wake, Daktari Bingwa wa Radiolojia kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Ramadhani Kabala, alisisitiza kuwa utekelezaji wa mpango huo utaongeza upatikanaji wa huduma za ultrasound katika ngazi za chini na kupunguza ulazima wa wagonjwa kusafiri umbali mrefu kufuata huduma katika hospitali za rufaa au za mikoa.
Mradi huu unatekelezwa na UDOM kwa ufadhili wa Gates Foundation, ukiwa na lengo la kuimarisha uwezo wa watumishi wa afya kupitia mafunzo ya matumizi ya Akili Unde katika huduma za sonografia. Hatua hii inatarajiwa kuboresha ubora wa huduma, kuongeza upatikanaji wake, na kuchangia mageuzi ya kidijitali katika sekta ya afya nchini.