UDOM YANG’ARA CHINA, KUIBUA FURSA MPYA ZA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA
Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kimeendelea kuimarisha nafasi yake kimataifa baada ya kuwasilisha miradi ya maendeleo, fursa za uwekezaji wa ubia kati ya sekta binafsi na umma (PPP), pamoja na maeneo mapya ya ushirikiano wa kimkakati katika mkutano maalumu uliowakutanisha viongozi wa Chuo Kikuu cha Zhejiang Normal na washiriki wa kimataifa wa Semina ya Taasisi za Kimataifa kutoka Afrika, inayoendelea katika mji wa Zhejiang, nchini China.
Katika wasilisho hilo, Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Umataifishaji, Jumuiya ya Wahitimu na Elimu Endelevu wa UDOM, Dkt. Godwin Myovella, alieleza dira na mipango ya Chuo katika kuendelea kupanua ushirikiano wa kimataifa kupitia miradi mbalimbali ya maendeleo, tafiti za pamoja, ubadilishanaji wa wanafunzi na watumishi, pamoja na matumizi ya teknolojia katika kuboresha ubora wa ufundishaji na ujifunzaji.
Dkt. Myovella alibainisha kuwa UDOM ipo katika hatua za kuanzisha Kampasi mpya ya Njombe itakayojikita zaidi katika masuala ya Kilimo, Biashara na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT), ikiwa ni sehemu ya mkakati wa Chuo wa kujitanua kitaifa na kimataifa katika kutoa elimu yenye kuendana na mahitaji ya maendeleo ya kisasa.
Aidha, alieleza kuwa Chuo kinaendelea kutekeleza Mpango Mkakati unaolenga kuifanya UDOM kuwa chuo cha kimataifa kinachozalisha wahitimu wenye ujuzi, ubunifu na ushindani katika soko la ajira la dunia. Sambamba na hilo, miradi mbalimbali ya ubia wa uwekezaji inayotarajiwa kutekelezwa kwa kushirikiana na wadau wa ndani na nje ya nchi, pia iliwasilishwa katika mkutano huo.
Akizungumza katika kikao hicho, Mkurugenzi wa Mahusiano ya Kimataifa wa Chuo Kikuu cha Zhejiang Normal ambaye pia alikuwa mwenyekiti wa mkutano huo, Prof. Mao Xilong, alisisitiza dhamira ya China kuendelea kuimarisha ushirikiano wake na nchi za Afrika kupitia elimu, utafiti, teknolojia na maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Prof. Xilong alieleza kuwa Chuo Kikuu cha Zhejiang Normal, kitapitia kwa kina maeneo yote yaliyowasilishwa na UDOM kwa lengo la kuanzisha ushirikiano wenye tija, matokeo halisi na manufaa ya muda mrefu kwa taasisi zote za Afrika zilizofanya Mawasilisho wakati wa mkutano huo. Aidha, alisisitiza kuwa China inaendelea kuweka mkazo katika ushirikiano wenye utekelezekaji na matokeo yanayoonekana, badala ya makubaliano yasiyo na utekelezaji wa vitendo.
Mafunzo hayo ya wiki mbili yameandaliwa na Chuo Kikuu cha Zhejiang Normal kwa ufadhili wa Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China, yakihusisha washiriki kutoka Tanzania, Namibia, Zimbabwe, Afrika Kusini, Lesotho na Gambia.
Kupitia semina hiyo, washiriki wamepata fursa ya kujifunza kuhusu mikakati na sera mbalimbali za China katika kuimarisha ushirikiano na mataifa ya Afrika katika maeneo ya uchumi, elimu, biashara, uzalishaji, teknolojia, pamoja na diplomasia na ushirikiano wa kimataifa. Ushiriki wa UDOM katika mafunzo hayo unaendelea kufungua milango mipya ya ushirikiano wa kimataifa, kubadilishana maarifa, pamoja na kuimarisha nafasi ya Tanzania katika mjadala wa maendeleo, elimu na ushirikiano wa kimataifa.