WANAFUNZI WA KIMATAIFA WANAOSOMA UDOM WAPEWA SEMINA


  • 2 weeks
  • The University of Dodoma

Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kupitia Kurugenzi ya Umataifishaji, Jumuiya wa Wahitimu na Elimu Endelevu, leo tarehe 9 Mei, 2025 wamewapatia semina maalumu wanafunzi wa kimataifa wanaosoma Shahada za Awali na Uzamili.

Akizungumza katika semina hii iliyofanyika katika jengo la Benjamin Mkapa (UDOM), Naibu Makamu Mkuu wa Chuo - Taaluma, Tafiti na Ushauri Elekezi (UDOM) Prof. Razack Lokina amesema, UDOM imeandaa mazingira mazuri na wezeshi na chuo kitaendelea kushirikiana nao ili kuhakikisha wanapata mafanikio kitaaluma.

Pia Prof. Lokina amewasihi wanafunzi hao kuwakaribisha wanafunzi wengine kutoka kwenye nchi zao, kuja kujiunga na (UDOM).

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Umataifishaji, Jumuiya ya Wahitimu na Elimu Endelevu (UDOM) Dkt. Lulu Kaaya amesema, wanaendelea kuboresha huduma wanazozitoa kwa wanafunzi wa kimataifa na kuhakikisha wanatatua changamoto zinazowakabili kwa wakati.

Naye, Afisa Uhamiaji Inspekta Izack Maganga, amewataka wanafunzi hao kuomba Viza na Kibali cha kuendelea kusoma hapa nchini kwa wakati, ili kuepuka usumbufu wowote unaoweza kujitokeza.

Mwakilishi wa Wanafunzi wa Kimataifa Bw. Fredy Oyoo amesema wanashukuru sana kwa kupatiwa semina hii kwani wamejifunza mengi na wanatumaini watazidi kuwa bora zaidi.

Pia wanafunzi hao walipata fursa ya kuelezewa zaidi kuhusu maswala ya bima ya afya, uhamiaji, ulipaji wa ada na umuhimu wa kujifunza lugha ya Kiswahili na Kiingereza.

Kikao hiki kilihudhuriwa na wageni mbalimbali kama vile Rasi wa Ndaki, Amidi na Wakurugenzi.

Comments
Send a Comment