UDOM NA BMH WASHIRIKIANA KUTOA MAFUNZO YA KUCHUJA DAMU


  • 2 weeks
  • The University of Dodoma

Chuo Kikuu cha Dodoma ( UDOM) kwa kushirikiana na Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) leo tarehe 12 Mei, 2025 wanafanya mafunzo ya njia sahihi ya kuchuja damu (fistula kwenye mkono) kwa wagonjwa wa figo ambayo yanafanyika katika Hospitali ya Benjamin Mkapa.

Akifungua mafunzo hayo, Mwakilishi wa Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma, Utafiti na Ushauri Elekezi Dkt. Jumanne Shakiru, amewataka washiriki kushiriki kikamilifu katika mafunzo hayo ili yaweze kuwa na tija katika utendaji wao.

“Aina hii ya mafunzo itawajengea uwezo wa kuwahudumia wagonjwa wa figo kwa kuzingatia viwango vilivyokusudiwa, hivyo basi; ni muhimu kushiriki kikamilifu ili mafunzo haya yaweze kuwa na tija". Amesema Dkt. Shakiru.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa, Dkt. Henry Humba, amewakaribisha washiriki wa mafunzo hayo BMH huku akieleza kuwa mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa ushirikiano uliopo kati ya UDOM na BMH.

“Hospitali ya Benjamin Mkapa imekuwa na ushirikiano mkubwa na uliodumu kwa miaka mingi na Chuo Kikuu cha Dodoma, leo tunafanya mafunzo haya ikiwa ni sehemu ya kuendeleza ushirikiano wetu na UDOM" Amesema Dkt. Humba.

Mafunzo hayo ambayo yanafanyika kuanzia tarehe 12 hadi 17 Mei, 2025 katika Hospitali ya Benjamin Mkapa yanahusisha washiriki 30 kutoka katika Hospitali ya Benjamin Mkapa, Chuo Kikuu cha Dodoma na Baadhi ya Hospitali za Mikoa wa Mkoa wa Dodoma.

Comments
Send a Comment