VIONGOZI WAPYA SERIKALI YA WANAFUNZI (UDOSO) WAAPISHWA
Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kimewaapisha viongozi wateule wa Serikali ya Wanafunzi chuoni hapa (UDOSO), leo tarehe 16 Mei, 2025 katika hafla fupi iliyofanyika katika Ukumbi wa Baraza (UDOM).
Akizungumza katika hafla hiyo, Makamu Mkuu wa Chuo (UDOM) amewapongeza viongozi wapya waliochaguliwa pamoja na wale wanaoondoka madarakani. Amesema viongozi hao watakuwa daraja kati ya Menejimenti ya Chuo na Wanafunzi.
Pia, anatarajia makubwa na mazuri zaidi kutoka kwa uongozi huu mpya kwani uliopita ulifanya vizuri sana kama uanzishwaji wa UDOSO Scholaship Bond.
"Uongozi sio kazi rahisi, lakini unakutambulisha kwenye jamii kwamba uko tayari kuwahudumia," aliongeza Prof. Kusiluka
Kwa upande wake, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma, Tafiti na Ushauri Elekezi Prof. Razack Lokina amewasihi viongozi hao wateule kuhakikisha wanahudhuria vipindi darasani kwani hilo ndilo jukumu lao kuu lililowaleta hapa chuoni. Pia amewataka kuwa na ushirikiano na menejimenti ya chuo pamoja na kusikiliza na kutatua changamoto za wanafunzi kwa wakati.
Aidha, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Mipango, Fedha na Utawala Prof. Albino Tenge amewataka viongozi hao wateule kuzingatia haki wakati wa kutekeleza majukumu yao, pamoja na kukakikisha wanadumisha amani na utulivu chuoni hapa.
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (UDOSO) Bi. Shamim Hussein Mganga amesema mchakato wa kuwapata viongozi wapya 2025/2026 haukuwa rahisi lakini kwa kushirikiana vizuri na menejimenti ya chuo, zoezi hili lilienda vizuri na limefanyika kwa ufanisi mkubwa.
Naye, Rais Mteule Bi. Jackline Humbaro ambaye mwaka aliopita 2024/2025 alikuwa Makamu wa Rais amesema watahakikisha wanatatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wanafunzi kwa kushirikiana na menejimenti ya chuo.
Hafla hii imehudhuriwa na viongozi mbalimbali kama vile Rasi wa Ndaki, Amidi wa Shule Kuu, Wakuu wa Taasisi, Walezi wa Wanafunzi, Katibu Mkuu wa TAHLISO, Wawakilishi kutoka Kitengo cha Ulinzi na Usalama pamoja na Viongozi wa Dini.