UDOM YATAKIWA KUPANUA UDAHILI WA MASOMO YA SAYANSI
Mwenyekiti wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), Prof. Makenya Maboko, ametoa wito kwa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kuongeza udahili wa wanafunzi katika masomo ya sayansi ili kukabiliana na uhaba wa wataalamu wa sayansi nchini.
Akizungumza wakati wa ziara ya Bodi ya TCU chuoni hapo leo, Machi 25, 2026, Prof. Maboko alisisitiza kuwa idadi ndogo ya wanafunzi wanaochagua masomo ya sayansi katika elimu ya juu haiendani na mahitaji halisi ya taifa katika sekta mbalimbali.
Alieleza kuwa upungufu wa wataalamu wa sayansi, hususan walimu wa masomo ya Fizikia, Hisabati na Kemia, bado ni changamoto kubwa ikilinganishwa na kada nyingine. Alisisitiza umuhimu wa kuongeza udahili sambamba na kuimarisha miundombinu ya kujifunzia na kuongeza idadi ya wahadhiri wenye sifa stahiki.
“Ni muhimu kuongeza idadi ya wanafunzi wa sayansi ili kujenga msingi imara wa wataalamu watakaokidhi mahitaji ya maendeleo ya Taifa,” alisisitiza Prof. Maboko.
Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Prof. Lughano Kusiluka, akitoa taarifa ya maendeleo ya chuo, alisema UDOM imepiga hatua kubwa katika maeneo ya ufundishaji, utafiti na ushauri elekezi.
Alibainisha kuwa chuo kimejijengea sifa mahsusi katika nyanja za Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) pamoja na afya, huku wanafunzi wake wakifanya vizuri katika mashindano ya kitaifa na kimataifa.
“Wanafunzi wetu wa TEHAMA wanaendelea kufanya vizuri sana, mara nyingi wakishika nafasi za juu katika mashindano mbalimbali. Kwa wastani, UDOM huchukua kati ya asilimia 80 hadi 90 ya nafasi za juu katika mashindano ya ICT wanayoshiriki,” alisema Prof. Kusiluka.
Aidha, aliishukuru Serikali kwa kuendelea kuwekeza katika kuboresha mazingira ya kujifunzia kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET). Kupitia mradi huo, UDOM inaendelea kujenga maabara katika Ndaki ya Sayansi Asilia na Hisabati, madarasa katika Ndaki ya Sayansi za Ardhi na Uhandisi, pamoja na kampasi mpya ya Njombe.
Alieleza kuwa uwekezaji huo utaongeza idadi ya wanafunzi wa sayansi na kuboresha ubora wa ufundishaji katika fani hizo.
Katika eneo la huduma kwa jamii, Prof. Kusiluka alieleza kuwa wanafunzi wa Shule Kuu ya Tiba na Afya ya Kinywa wanaofanya mafunzo kwa vitendo katika hospitali mbalimbali, hususan Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa, wamekuwa wakitoa mchango mkubwa katika utoaji wa huduma bora za afya.
Ziara ya Bodi ya TCU ni sehemu ya jukumu la Tume la kufuatilia na kutathmini maendeleo pamoja na changamoto za taasisi za elimu ya juu nchini. Katika ziara hiyo, wajumbe wa Bodi walitembelea Shule Kuu ya Tiba na Afya ya Kinywa, Ndaki ya Sayansi za Kompyuta na Elimu Angavu, pamoja na Hospitali ya Chuo Kikuu cha Dodoma.