WALIMU KIBAIGWA WAPEWA MBINU BUNIFU ZA KUFUNDISHA MASOMO YA SAYANSI


  • 6 hours
  • The University of Dodoma
Walimu wa shule za sekondari kutoka mikoa ya Dodoma na Simiyu wanashiriki mafunzo ya Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati (STEM) yanayofanyika katika Shule ya Sekondari Mt. Pio, Kibaigwa wilayani Kongwa, yakilenga kuwajengea uwezo wa kutumia mbinu bunifu za ufundishaji ili kuboresha ufaulu wa wanafunzi.
 
Akifungua rasmi mafunzo hayo, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo anayeshughulikia Taaluma, Tafiti na Ushauri Elekezi wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Profesa Razack Lokina, alisisitiza umuhimu wa ushirikiano katika kuimarisha elimu ya sayansi.
 
“Mafanikio ya masomo ya STEM hayategemei mwalimu pekee, bali ni matokeo ya juhudi za pamoja kati ya walimu, taasisi za elimu na wadau wote wa elimu,” alisema Prof. Lokina.
 
Aliongeza kuwa uwekezaji kwa walimu ni nguzo muhimu katika maendeleo ya elimu ya sayansi nchini, akikazia umuhimu wa kuwawezesha Walimu mbinu bora na bunifu za kufundishia ili kuzalisha kizazi chenye uwezo wa kufikiri vema.  
 
Kwa upande wake, mmoja wa walimu washiriki kutoka mkoa wa Simiyu alisema mafunzo hayo yameleta mabadiliko chanya katika mtazamo wao wa ufundishaji.
 
“Mafunzo haya yametufungua macho. Sasa tunaona namna ya kuwafanya wanafunzi washiriki kikamilifu badala ya kufundisha kwa maelezo ya kawaida pekee,” alisema.
 
Aidha, Chuo Kikuu cha Dodoma kimeeleza kuwa kitaendelea kushirikiana na walimu kwa kutoa mafunzo zaidi yatakayosaidia kuboresha mbinu za ufundishaji na kuinua kiwango cha ufaulu wa wanafunzi katika masomo ya sayansi nchini.
 
Mafunzo hayo ni sehemu ya jitihada endelevu za kuimarisha ubora wa elimu ya sayansi nchini, yakilenga kuwajengea walimu uwezo wa kutumia mbinu shirikishi na zinazomlenga mwanafunzi darasani, hatua inayotarajiwa kuongeza uelewa na ufaulu katika masomo ya STEM.
Comments
Send a Comment